KF 203 : FASIHI YA WATOTO NA VIJANA. UTANGULIZI:
Ni vyema kuanza kufafanua maana za maneno
mbalimbali ya msingi yaliyojitokeza katika kauli hii kama vile: maana ya fasihi
kwa ujumala, maana ya fasihi ya watoto na vijana, maana ya fasihi ya watu
wazima pamoja na maana ya mipaka. Baada ya hapo kiini cha mada, ambapo tutaona
ukubalifu wa hoja, kisha zitafuata sababu zinazoonesha ugumu wa kuweka mipaka
dhahiri kati ya fasihi ya watoto na vijana na ya watu wazima.
Mulokozi (1996) anafafanua kuwa fasihi ni
sanaa ya lugha inayoangalia maisha na mazingira halisi ya mwanadamu kwa kutumia
lugha na maandishi
Kwa mujibu wa Ngure (2003:1) fasihi ni aina ya
sanaa ambayo wasanii wake huonesha ustadi wao katika kutumia maneno kisanaa ili
kuwasilisha ujumbe wao kwa wasomaji/jamii iliyonuiwa.
Pia Mulokozi (ameshatajwa) akimnukuu Egletoni
(1983:20-21) fasihi ni sanaa ya lugha yenye ubunifu bila kujali kama imeandikwa
au la.
Vilevile Nkwera (1978) anafafanua kwamba,
fasihi ni sanaa yaani mkusanyiko wa kazi mbalimbali zilizosanifiwa kwa kutumia
lugha itumiayo zaidi maneno, na kujishughulisha na jinsi binadamu
anavyojitambulisha mwenyewe binafsi, pia anavyoathiriwa na binadamu wenzake
aidha na viumbe vingine aina kwa aina katika mazingira mbalimbali ya maisha.
Hivyo kutokana na fasili hizo, kwa kifupi maana
ya fasihi ni kazi ya sanaa inayotumia lugha katika kufikisha ujumbe kwa hadhira
husika.
Wamitila (2003) anafafanua fasihi ya watoto
kuwa ni fasihi maalum inayoandikwa kwa ajili ya watoto. Hii ni fasihi ambayo ni
tofauti na ngano au hurafa.
Hivyo fasihi ya watoto na vijana ni kazi ya
sanaa inayotumia lugha ilikufikisha ujumbe kwa watoto na vijana ambao wanaumri
chini ya miaka 18.
Fasihi ya watu wa zima ni kazi ya sana inayotumia
lugha ilikufikisha ujumbe kwa watu wenye umri juu ya miaka 18.
Kamusi ya kiswahili sanifu (2004) inafafanua
maana ya mpaka kuwa ni mahali ambapo kikomo cha kitu na kingine.
Hivyo dhana ya mpaka inaweza kufasiliwa kuwa
ni dhana inayoonesha mwachano baina ya kitu kimoja na kingine. Kwa mfano,
inaweza kuwa mpaka kati ya nchi na nchi au eneo moja na jingine na hata kitu
kimoja na kingine.
Ni kweli kabisa kuwa ni vigumu kuweka mipaka
dhahiri kati fasihi ya watoto na vijana na fasihi ya watu wazima. Na hii
inatokana na sababu za mwingiliano katika vipengele mbalimbali kama vile:
Muundo wa matini. Katika fasihi kuna miundo
mbalimbali, kwa mfano, muundo changamani, muundo sahili na muundo rejea. Hivyo
basi, ni suala la kawaida kukuta muundo wa moja kwa moja ambao ndiyo msingi wa
fasihi ya watoto na vijana katika fasihi
ya watu wazima. Kwa mfano, riwaya ya “Vuta N’kuvute” ya Shaffi Adam Shaffi visa
vyake vimepangangwa kwa mtiririko wa moja kwa moja.
Wahusika na uhusika. Hoja hii inajitokeza
katika fasihi zote mbili yaani fasihi ya watoto na vijana na fasihi ya watu
wazima, ambapo kwenye fasihi ya watoto na vijana kuna wahusika ambao ni watu
wazima wenye kuvaa uhusika wa watoto yaani sehemu ambapo ilitegemewa awepo
mhusika mtoto anawekwa mtu mzima, kadhalika kwa upande wa fasihi ya watu wazima
hali hii hujitokeza pia. Kwa mfano katika tamthiliya “Wala Mbivu” ilipoigizwa
kwa mara ya kwanza mwaka 1971 ambapo wahusika walioigiza walivaa uhusika wa
watu wazima, mfano, wapo walioigiza kama baba, mama, mjomba, na shangazi,
Matumizi ya fantasia. Fantasia ni hali ya
kuwepo kwa mambo ya ajabuajabu katika kazi ya fasihi yasiyotarajiwa kutokea
katika maisha ya kawaida. Hali hii inajitokeza katika fasihi zote mbili yaani
fasihi ya watoto na vijana na fasihi ya watu wazima. Kwa mfano katika tamthiya
ya “Kivuli Kinaishi” matumizi ya fantasia yametumika kwa kiasi kikubwa ambapo
ilitegemewa dhana hii ijitokeze katika fasihi ya watoto na vijana ambayo ni
moja ya sifa kuu ya kazi hizo. Hivyo ugumu unajitokeza katika kujua fantasia ni
dhana ya watoto au watu wa wazima.
Mwingiliano katika usomaji. Mara kwa mara
wasomaji wa kazi hizi huingiliana yaani unakuta kazi zinazohusu watoto husomwa
na watu wazima halikadhalika kazi za watu wazima husomwa na watoto. Hii
inatokana na kutokuwepo kwa maktaba za kutosha za kazi za watoto. Pia hali hii
inasababishwa na kukosekana kwa sheria zinazoweka mipaka kati ya kazi hizi. Hivyo
inakuwa vigumu kuzuia mwilingiliano huu.
Mwingiliano katika mtindo. Mara nyingi baadhi
ya vipengele vya kimtindo vya fasihi ya watoto na vijana hujitokeza hata katika
fasihi ya watu wazima. Kwa mfano, matumizi ya picha mbalimbali zenye kufafanua
maelezo ya mwandishi hujitokeza katika fasihi zote mbili. Mfano, katika riwaya
ya “Mfadhili” ya Hussein Tuwa, pamoja na tamthiliya ya “Aliyeonja Pepo” ambazo
ni fasihi za watu wazima waandishi wametumia picha mbalimbali katika kuelezea
visa vyao. Hivyo matumizi ya picha pamoja na michoro ni kipengele muhimu katika
fasihi ya watoto na vijana ambacho huwasaidia watoto kuelewa zaidi na kuvutiwa.
Vilevile uwepo wa matumizi ya taharuki. Dhana
hii ina maana kwamba ni hali ya wasomaji kuwa na mshawasha wa kutaka kujua ni
kitu gani kitafuata katika mwendelezo wa kisa. Dhana hii hujitokeza katika kazi
zote mbili, hivyo inaleta ugumu katika kujua dhana hii inaangukia wapi kati ya
fasihi ya watoto na vijana au fasihi ya watu wazima.
Kadhalika ni vigumu kubaini mawazo au falsafa
ya mtunzi. Hii ni kutokana na kwamba kazi nyingi za kifasihi hutungwa na watu
wazima zikiwemo pia kazi za watoto na vijana. Hivyo kuna kuwa na mwingiliano mkubwa wa mawazo na
kushindwa kubaini yapi ni mawazo ya watoto na yapi ni ya watu wazima.
Hivyo basi ili hali hii ya mwingiliano iweze
kuepukika ni dhahiri kwamba kunahitajika kuwepo kwa sheria madhubuti na zenye
kutekelezeka zitakazo dhibiti kazi hizi mbili zisiweze kuingiliana, hasa kwa
watunzi na wasomaji. Kwa mfano watunzi wa fasihi ya watoto na vijana wajikite
katika fasihi hiyo tu na watunzi wa fasihi ya watu wazima wajikite katika
fasihi ya watu wazima tu na wala kusiwepo na mwingiliano wowote wa vipengele ili
kuwapa urahisi wasomaji kujua mipaka ya kazi hizo.
MAREJEO.
Nkwera,
F.V. M. (1978), Sarufi Fasihi: Uandishi
wa Vitabu Sekondari na Vyuo. Tanzania publishing House. Tanzania.
Ngure, A. (2003),FasihiSimulizikwaShulezaSekondari.
Nairobi. Phoenix Publisher.
OUP (T). Ltd. East African & TUKI. (2004),
Kamusi ya Kiswahili Sanifu. (Toleo la pili). Oxford University Press (T). Ltd.
Mulokozi,
M.M. (1996), Utangulizi wa Fasihi ya Kiswahili. Taasisi ya Uchungu wa Kiswahili. Dar es
Salaam.
Wamitila,
K.W. (2003), Kamusi ya Fasihi na Nadharia.
Focus Publication Ltd. Nairobi-Kenya.
No comments:
Post a Comment