OSW 122. HISTORIA YA KISWAHILI NA LAHAJA ZAKE.
Kiswahili ni lugha ya Kibantu yenye misamiati mingi ya Kiarabu inayozungumzwa katika eneo kubwa la Afrika ya Mashariki.Lugha hii ina utajiri mkubwa wa misamiati, misemo, mithali, mashairi, mafumbo, vitendawili na nyimbo. Kiswahili hutumika mashuleni na kuna vitabu vingi vilivyotungwa kwa kutumia lugha hiyo, vikiwa pamoja na vile vya hadithi, hekaya au riwaya.
Yaliyomo
Historia ya lugha
Inaonekana ya kwamba lugha mpya ilijitokeza wakati wenyeji wa pwani, waliokuwa wasemaji wa lugha za Kibantu, walipopokea maneno mengi hasa ya Kiarabu katika mawasiliano yao. Kwa hiyo msingi wa Kiswahili ni sarufi na msamiati wa Kibantu pamoja na maneno mengi ya Kiarabu. Imekadiriwa ya kwamba theluthi moja ya maneno ya Kiswahili yana asili ya Kiarabu.
Kando ya Kiarabu kuna pia athira ya lugha mbalimbali kama Kiajemi, Kihindi na Kireno. Wakati wa karne ya 20 maneno mengi yalipokewa kutoka Kiingereza.
Kwa karne nyingi iliandikwa kwa herufi za Kiarabu (سواحلي sawaHili au لغة سواحيلية lugha sawaHiliya).
Sarufi ya kwanza pamoja na kamusi iliandikwa mwaka 1848 na Dr. Ludwig Krapf huko Rabai Mpya / Mombasa.
Kiswahili kilikuwa na lahaja nyingi kutokana na lugha mbalimbali za Kibantu zilizochangia mle.
Tangu karne ya 19 lugha ilianza kuenea barani kwa njia ya biashara.
Wakati wa ukoloni wa Uingereza lugha ilisanifishwa kwa njia ya Kamati ya kimaeneo ya lugha ya Kiswahili kwenye msingi wa lahaja ya Unguja.
Wasemaji
Hakuna hakika kuhusu idadi ya wasemaji wa lugha hiyo; idadi zinazotajwa zinatofautiana. Wasemaji wanaoitumia kama lugha ya kwanza hawapungui milioni 10, na wasemaji wanaoitumia kama lugha ya pili ni zaidi ya milioni 70.Idadi ya wasemaji wa lugha ya kwanza inakua haraka, kwa sababu lugha inaenea katika maeneo ambapo lugha nyingine zilikuwa lugha kuu, na hasa katika miji ya Tanzania imekuwa lugha kuu, badala ya lugha za kikabila, kutokana na mchanganyiko wa watu hata ndani ya nyumba, kama vile wanapooana watu wa makabila tofauti, jambo ambalo limekuwa la kawaida hasa Tanzania, ambayo inaongoza kwa matumizi ya Kiswahili.
Kati ya nchi nyingine ambapo Kiswahili kinatumika kuna Kenya, Uganda, Kongo-Kinshasa, Rwanda, Burundi, Msumbiji, Somalia na visiwa vya Bahari Hindi kama Visiwa vya Ngazija (Komoro).
Lugha rasmi
Kiswahili kimekuwa lugha rasmi katika nchi zifuatazo:- Tanzania: ni lugha ya taifa; ni lugha ya shule za msingi, lugha ya utawala serikalini na mahakamani; inatumika kote nchini, makanisani, misikitini, redioni, kwenye runinga na idadi kubwa ya magazeti.
- Kenya: ni lugha ya taifa lakini Kiingereza ni lugha rasmi ya kiutawala; Kiswahili ni lugha ya kwanza ya mawasiliano kati ya wananchi wakikutana nje ya eneo lenye kabila moja tu; ni lugha inayofundishwa lakini si lugha ya kufundisha mashuleni; ni lugha inayotumika na polisi na jeshi, ni lugha ya kuhutubia wananchi mjini na kitaifa; sehemu za ibada makanisani zinatumia Kiswahili; kuna gazeti moja tu la Kiswahili; sehemu za programu redioni na kwenye runinga ni kwa Kiswahili. Lugha inachanganywa mara nyingi na Kiingereza na lugha za maeneo au za kikabila. Hata hivyo baada ya rasimu ya katiba mpya kupitishwa tarehe 4 Agosti 2010, Kiswahili sasa kitakuwa lugha rasmi, sawa na Kiingereza.
- Uganda: kimetangazwa kuwa lugha ya kitaifa tangu 2005; iliwahi kuwa lugha ya kitaifa wakati wa utawala wa Idi Amin; wakati wa ukoloni ilifundishwa mashuleni ikaelekea kuwa lugha rasmi pamoja na Kiingereza lakini matumizi haya yalipingwa hasa na Waganda hivyo Waingereza waliacha mipango hiyo. Ni lugha ya polisi na jeshi, hali ambayo imeleta ugumu kwa lugha kukubalika na wananchi wengi kutokana na historia ya utawala wa kijeshi Uganda; watu wengi bado hukumbuka hasa matusi ya wanajeshi waliowatesa wakisema Kiswahili. Lakini kuna maeneo ya Uganda ambako Kiswahili kinatumiwa na watu wengi kama lugha ya sokoni na barabarani. Wona UBC, WBS tv.
- Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo: Kiswahili ni kati ya lugha nne za kitaifa, pia lugha ya jeshi katika mashariki ya nchi. Kiswahili kimefika na misafara ya biashara ya watumwa na pembe za ndovu kutoka Zanzibar na pwani ya Tanganyika. Imeenea zaidi kati ya mchanganyiko wa wafanyakazi kwenye migodi ya Shaba.
Lugha ya kwanza, lugha ya pili
Kiasili Kiswahili kilikuwa lugha ya kwanza tu ya wakazi wa miji ya Waswahili kwenye pwani, katika sehemu za pwani pia kijijini. Baada ya kuenea kimekuwa lugha ya watu wengi mjini hasa Tanzania lakini pia Kenya.Kimeenea zaidi kama lugha ya mawasiliano na biashara pale ambako watu wa makabila mbalimbali wanakutana. Pamoja na nchi zinazotajwa hapo juu Kiswahili kinatumika katika Kaskazini ya Msumbiji, Kusini kabisa ya Somalia, Mashariki ya Burundi.
Maeneo ya mpaka wa Tanzania kuna pia wasemaji kadhaa huko Malawi na Zambia.
Tanzania na Kenya zilipokea wakimbizi wengi waliojifunza Kiswahili lakini hakuna uhakika kama bado kinatumika wakirudi Rwanda, Sudan au Somalia.
Kimataifa
Lugha hii leo imekuwa na umuhimu mkubwa duniani kwa jumla, na hasa Africa, kwa sababu ya kuenea kwake nchi mbali mbali, na kukusanya kwake watu wa makabila na nchi kadha wa kadha wakaweza kufahamiana kwa lugha moja, hasa ilivyokuwa ni lugha mojawapo katika lugha kubwa za Africa ambazo zinachukuwa mahala pa lugha za kigeni na Wakoloni, kama Kiarabu, Kiurdu, Kiebrania, Kireno na kadhalika.Leo, imekuwa inatumiwa katika kusambaza habari katika vituo mbali mbali ulimwenguni kama vile Sauti ya Amerika, BBC, Deutsche Welle, Monte Carlo, na nchi nyinginezo za Uchina, Urusi, Irani na kwengineko.
Aidha, imekuwa ni mojawapo ya lugha muhimu zinazofundishwa katika vyuo vikuu nchini Marekani, Uingereza, Ulaya bara, Urusi, Uchina, na barani Afrika.
Maendeleo ya Kiswahili
Lugha ina maendeleo: inaweza kukua, kukwama au kufa. Athira nyingi hutokea bila mpangilio pale ambako wasemaji wanapokea maneno mapya, wanaacha kutumia maneno mengine au hubadilisha kawaida ya matamshi au sarufi. Haya yote hutokea pia katika uwanja wa Kiswahili.Kuna mzaha unaosimuliwa hasa Tanzania: Kiswahili kilizaliwa Unguja, kilikua Tanzania Bara, kikafa Kenya na kuzikwa Uganda. Hali halisi Kiswahili kina maendeleo yake katika nchi hizo zote labda zaidi Kongo.
Lakini itategemea pia juhudi za serikali kama umoja wa lugha utatunzwa kwa sababu kuna athari nyingi kutoka lugha za kila eneo zinazoingia katika ukuzi wa Kiswahili kwa namna zinazotofauitiana.
Taasisi zinazokuza Kiswahili
Kuna taasisi zinazolenga kukuza na kuimarisha Kiswahili kama vile Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI) kwenye Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pamoja na idara za Kiswahili katika vyuo vikuu vingine vya Kenya na pia Uganda.Nchini Tanzania kuna Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) na Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) ilhali nchini Kenya kuna Chama cha Kiswahili cha Taifa (CHAKITA). BAKITA na CHAKITA pamoja na wawakilishi kutoka Uganda wanaandaa kuundwa kwa Baraza la Kiswahili la Afrika Mashariki (BAKAMA).
Uchunguzi wa Kiswahili huendelea pia katika idara za vyuo vikuu vingi duniani, kwa mfano katika Institute National des Langues et Civilisations Orientales, mjini Paris, Ufaransa. Matumizi yake ni kwa njia ya lahaja za Kingwana.
Kamusi za Kiswahili
Tazama pia
- Historia ya Kiswahili
- Lahaja za Kiswahili
Lahaja
Lahaja ni vilugha vidogovidogo vya lugha moja ambavyo hubainika kijamii au kijiografia. Lahaja za lugha moja zatofautiana katika matamshi, miundo ya sarufi na msamiati. Kama lugha hutofautiana katika matamshi tu, tofauti hizo huitwa lafudhi na siyo lahaja. Uchambuzi na uchanganuzi wa lahaja ni tawi la isimujamii.
Lahaja hutofautishwa kulingana na vipengele vifuatavyo:
- vipengele vya sera (lahaja rasmi na lahaja sanifu)
- vipengele vya maoni ya wasemaji wa lugha husika (k.m. lahaja maarufu)
- vipengele vya kijamii (lahaja jamii na lahaja tabaka)
- vipengele vya eneo (kitarafa)
Marejeo
- TUKI 1990, "Kamusi Sanifu ya Isimu na Lugha", Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
- Massamba, David 2004, "Kamusi ya Isimu na Falsafa ya Lugha", Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
- Buliba, Aswani, Kimani Njogu & Alice Mwihaki 2006, "Isimujamii kwa Wanafunzi wa Kiswahili", Nairobi: The Jomo Kenyatta Foundation
Tazama pia
Makala hii kuhusu mambo ya lugha bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Lahaja kama historia yake, uenezi au maendeleo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.