Monday, 28 April 2014

KF 302 :FASIHI SIMULIZI YA KISWAHILI NA KIAFRIKA.

KF  302 :FASIHI SIMULIZI YA KISWAHILI NA  KIAFRIKA.



SWALI: FASIHI SIMULIZI YA KIBANTU INGEWEZA KUWA NI RASLIMALI MUHIMU 

fafihi simulizi ya kiswahili



KWA MAENDELEO YA JAMII. BAINISHA AMALI ZINAZO AKISIWA NA KABILA LA KIBANTU ZA TANZANIA NA VIPENGELE MUHIMU VYA UHUSIANO WAKE KATIKA MAENEO MBALIMBALI YA JAMII KWA KUZINGATIA MUKTADHA MPANA WA UTANDAWAZI. MIFANO IJIKITE KATIKA KABILA LA WASAFWA NA WANYAKYUSA

Fasihi simulizi kama dhana, imeelezwa na wataalamu wengi kwa kutegemea nadharia na mitazamo mbalimbali , hata hivyo ni muhimu kufahamu ya kwamba maana inayopewa dhana au kitu fulani, huwa inachukuana na matumizi ya dhana yenyewe, watu wanaohusika, mahali dhana hiyo inapotokea na hata kipindi au wakati husika. Hii ndio sababu tunapata fasili mbalimbali zinazorejea dhana ya fasihi simulizi kama ifuatavyo:

Ngure, A.(2003), anafasili fasihi simulizi kama sanaa itoayo maudhui yake kwa lugha ya maneno ambayo hutamkwa ama kutendwa. Kwa mijibu wa maana hii, Ngure anasisitiza kwa kusema fasihi ni namna ya utoaji wa maudhui kisanaa na kuwasilishwa kwa njia ya mdomo ambayo huweza kutamkwa au kutendwa.

Mulokozi (1996:24) anasema, fasihi simulizi ni fasihi inayotendwa au kubuniwa kichwani na kuwasilishwa kwa hadhira kwa njia ya mdomo na vitendo bila kutumia maandishi, hivyo fasihi simulizi ni tukio linalofungamana na muktadha (mazingira) fulani wa kijamii na kutawaliwa na mwingiliano wa fanani, hadhira, fani inayotendwa, tukio, mahali na wakati. Mulokozi anafafanua kwa kusema fasihi simulizi ni ile fasihi inayotendwa au kubuniwa kichwani na kuwasilishwa kwa njia ya mdomo ikiambatana na vitendo, swali ni kwamba fasihi simulizi inayowasilishwa kwa njia ya redio, tepurekoda pamoja na luninga sio fasihi simulizi?
Finnegan (1970) anaeleza kuwa fasihi simulizi ni sanaa ambayo hutegemea msanii ambaye huiumba kwa maneno katika tukio maalumu. Katika fasili hii Finnegan hajagusia mambo muhimu katika fasihi simulizi kama vile muktadha, namna ya uwasilishaji, uhifadhi na badala yake amejikita zaidi katika ubunifu alionao msanii anayeiumba fasihi husika.  

Balisidya (1983) anafasili fasihi simulizi kama aina ya fasihi ambayo hutumia mdomo katika kuiumba, kuiwasilisha na kusambazwa kwa wasikilizaji na watumiaji wake. Fasili hii ina mapungufu kwani haijafafanua juu ya ubunifu alionao msanii katika kuikamilisha, na pia katika suala la uwasilishaji tunaweza kujiuliza kwamba je, fasihi simulizi lazima iwasilishwe kwa njia ya mdomo tu?
Hivyo basi, kutokana na fasili zote hapo juu tunaweza kufasili fasihi simulizi kuwa ni kazi ya sanaa inayotumia mazungumzo ya ana kwa ana ikihusisha utendaji na njia nyingine za mawasiliano kama vile tepurekoda, redio, luninga na vinginevyo ili kufikisha ujumbe kwa jamii husika.
Kuna tanzu nyingi za fasihi simulizi kutokana na wataalamu tofauti kuwa na mawazo tofauti tofauti, tanzu hizo zimewekwa katika makundi au tanzu kuu nne ambazo ni hadithi, semi, maigizo na ushairi.

TUKI (2004) wanafasili amali kuwa ni matendo, kazi na mazoea, hivyo kwa maelezo hayo amali za jamii ni jumla ya mazoea, kazi mbalimbali na matendo yote yanayofanyika katika jamii husika kama vile mila na desturi, utamaduni, dini, siasa na uchumi.
www.wikipedia.org/wiki, wanafasili amali za jamii kama tawi la isimu ambalo huchunguza uhusiano kati ya lugha na jamii, aidha inajihusisha na athali yoyote ya jamii kama vile desturi za watu, matazamio na muktadha katika nyanja za lugha na namna inavyotumika.
Hivyo, amali za jamii huhusisha tamaduni, mila, desturi, dini, siasa na uchumi na haya yote sharti yahifadhiwe katika uasili wake ambapo hutunzwa, huhifadhiwa, kulindwa na kuendelezwa na fasihi simulizi.
Matumizi ya utandawazi yalianzia miaka ya tisini yakimaanisha kukifanya kitu kuwa katika kiwango cha kimataifa na kukifanya kuwa wazi na kufanywa na watu wa aina yoyote duniani (www.wikipedia.org/wiki/isimu).
Kutokana na fasili hii, utandawazi unaweza kuelezwa kama njia ambayo wenyeji au taifa hufanya mambo kuwa ya kimataifa na unahusu suala zima la uchumi, biashara, teknolojia, siasa na utamaduni.
Wasafwa na Wanyakyusa ni miongoni mwa makabila ya kibantu yanayopatikana nchini Tanzania mkoani Mbeya.

Kabila la Wasafwa hupatikana katika wilaya ya Mbeya mkoani Mbeya, jamii hii inajishughulisha na kilimo pamoja na ufugaji. Shughuli hizi ndizo zinazofanya amali zao zitofautiane na amali za jamii nyingine.
Kabila la wanyakyusa hupatikana katika wilaya za Rungwe na Kyela katika mkoa wa Mbeya, jamii ya wanyakyusa hufanya shughuli mbazo hutofautiana kulingana na sehemu wanakotoka (yaani mazingira). Wanyakyusa wa Rungwe hujishughulisha na kilimo na ufugaji na wale wa Kyela hujishughulisha na kilimo, ufugaji na uvuvi.

Ingawa makabila haya hupatikana katika wilaya husika yaani Wasafwa kwa wilaya ya Mbeya na Wanyakyusa wilaya ya Rungwe na Kyela, shughuli za utafutaji mali zimesababisha jamii ya Wanyakyusa na Wasafwa wapatikane sehemu nyingine pia za nchi ya Tanzania.
Amali mbalimbali zinazopatikana katika makabila ya kibantu ni pamoja na mila na desturi, utamaduni, dini (imani), siasa na uchumi.

Utamaduni ni jumla ya mambo yote yanayobuniwa na jamii ili kukidhi utashi na maendeleo yake (Mwambusye, 2013). Katika fasili hii mambo yanayozungumziwa ni ndoa, uzazi, malezi, marika, mafunzo mbalimbali ya mazingira na shughuli zingine kama jando, ngoma na imani katika Mungu, miungu, mashetani na mizimu, vyakula, mavazi, mapambo, salamu na lugha.
Utamaduni ni mojawapo ya nyenzo muhimu ya maendeleo katika jamii yoyote ile kama amali mojawapo ya jamii, tamaduni zilikuwa sharti zibaki katika uasili wake katika vipengele vya muktadha, wahusika, maudhui, hadhira na fanani.

Suala la ndoa katika kabila la wasafwa waliohusika kumfundisha mwali ni shangazi na bibi ambao hasa walikuwa ndio fanani, mwali huyo alifundishwa namna ya kuishi katika ndoa pamoja na matumizi mazuri ya chakula katika familia, kwa mfano binti alifundishwa kupika chakula ambacho kingetosheleza mahitaji ya mumewe na familia yake kwa ujumla bila kubakiza na kukitupa. Katika shughuli hii mwali ndiye aliyekuwa hadhira na ukweni ndio palikuwa mahali pa kutendea na maudhui yalikuwa ni mafunzo kuhusu maisha ya ndoa na fanani walikuwa bibi na shangazi wa mwali, katika kipindi hicho mafunzo hayo yalimfundisha mwali namna ya kuishi na jamii inayomzunguka na mafunzo yote yalifikishwa kwa njia ya misemo, nyimbo na hadithi. Mfano wa nyimbo zilizokuwa zikiimbwa wakati wa mafunzo hayo ni kama vile:
                                         “Wamala yashi ingano
                                           yaleta bana yao
                                           yenye ubaba ni mama
                                           bayinzilile mwigomba”.
Wimbo huu ulimfundisha mwali kutokumaliza chakula ndani kwa ajili ya matumizi ya baadaye na kwa ajili ya wageni.

Kutokana na maendeleo ya utandawazi amali hii imepoteza uasili wake kutokana na kuathiriwa katika uwasilishaji wake, fanani yake, mahali pa kutendea na hata maudhui yake yaani mafunzo hayo katika muktadha wa utandawazi huitwa “Kitchen party” au sherehe ya jikoni (tafsiri yetu) ambayo hufanyika kwenye kumbi na fanani huwa mtu yeyote sio wale wa asili na maudhui pia yamebadilika kwani yaliyofundishwa kipindi katika kipindi kile sio yanayofundishwa leo. Hivyo amali hii imepoteza thamani yake ya kuwa rasilimali muhimu kwa maendeleo ya jamii.

Kimsingi katika ndoa za kinyakyusa wazazi ndio waliohusika kuwachagulia wenzi wa ndoa vijana wao, suala la utoaji wa mahari ilikuwa ni sehemu ya amali ya jamii kwa kabila la Kinyakyusa. Ili kuhakikisha usalama wa binti wa kinyakyusa bibi au shangazi waliwachunguza mabinti zao mara kwa mara mpaka siku ya ndoa, mchakato huo ulizua misemo mingi kwa mfano mzazi angeweza kumwonya binti yake ajitunze kwa kusema “Api kujoba pa kijinja” yaani heshima na mambo yako yatathibitika penye migomba.  “Pa kijinja” palikuwa ni mahali ambapo binti alipelekwa kwa uchunguzi ili kuthibitisha ubikra wake hivyo kitendo cha kumchunguza kiliitwa “Ukosya” yaani kuoshwa. Endapo binti akigundulika kuwa alishaingiliwa kimwili ilisemwa kuwa “inguku jiligilwe” yaani kuku ameliwa, hii ilisababisha binti kutolewa mahari ndogo yaani ng’ombe wachache ikilinganishwa na binti ambaye alikutwa salama yaani hajaingiliwa na wanaume yaani aliyekutwa ni bikira ambaye mahari yake ilikuwa ni kubwa. Kutokana na umuhimu huo, mabinti walilazimika kujitunza mpaka siku ya ndoa,  hali iliyosababisha mahari kuwa kubwa na heshima kwa familia husika na fahari kwa ukoo wa mwanaume.
Kwa upande wa jamii, hali hii ilisaidia wanawake kutokuchezewa na kutozaa watoto nje ya ndoa yaani “isigwana”, kwa hali hiyo uchumi wa wazazi wa binti uliongezeka pamoja na heshima  ya binti na jamii kwa ujumla.

Kutokana na utandawazi, mfumo wa elimu kuwapeleka watoto shule na mwingiliano wa tamaduni umesababisha wanyakyusa kuoana na makabila mengine,  hivyo  kusababisha amali hii kuathiriwa na utandawazi kwa kuwa hakuna tena utaratibu wa kuwakagua mabinti yaani “Ukosya”,  pia utaratibu wa kutoa mahari nao umebadilika kwani mahari ya kutoa ng’ombe imekuwa ikithaminishwa na fedha taslimu.
Hivyo basi, katika kipindi hiki baadhi ya wazazi wamekosa mahari ambazo zingewasaidia kuendesha shughuli zao za maendeleo kutokana na watoto wao kujioza wenyewe na kusababisha mahali kuwa kidogo na hivyo kuifanya amali hii kama kipengele muhimu cha fasihi simulizi kupungukiwa thamani ya kuwa rasilimali muhimu katika maendeleo ya jamii kwa ujumla.

Tambiko ni utekelezaji wa ada maalumu ili kutuliza mizimu, koma au pepo, sadaka edaha, kafara, mviga, miiko (TUKI, 2004). Hivyo tambiko ni sadaka itolewayo kwa mwenyezi Mungu au miungu kwa lengo la kuomba au kumshukru kwa mambo mbalimbali yanayoikabili jamii. Tambiko katika jamii ya wasafwa ilihusisha matukio mbalimbali katika jamii kama vile magonjwa, njaa, ukame, mashambulizi ya wanyama au maadui ambavyo viliaminiwa kutokana na kuwaudhi mizimu au miungu.  Unyeshaji wa mvua kwa wakati na kiasi cha kutosha ulikuwa ni muhimu sana wakati ukame ulipotokea. Kiongozi mkuu huongoza kundi la wazee kwenda “Iganjo” yaani mahali pa kutambikia wakiwa na pombe ndani ya vibuyu vitano au sita pamoja na kuku mweusi. Siku maalumu hutangawa kwenda kuomba mvua hivyo hakuna mwanajamii anayeruhusiwa kufanya kazi yoyote. Mwene ndiye kiongozi wa ibada kwa kusihi mizimu, mfano “uposhele inguku ini, tuhanzaje hunzi hwilwepei invula itonye”, maana yake “Pokea kuku huyu tunataka nchini kuwe kweupe akiomba mvua inyeshe”.
Baada ya hapo wazee humchoma kuku akiwa na manyoya yake mpaka aive na humla na kunywa pombe. Ibada ziliweza pia kuuliza neno gumu na kushukru kwa mambo mazuri waliyoyapata. (http://www.safarilands.org/docs/jamii-ya-wasangu-tanzania.pdf).
Kwa upande wa kabila la wanyakyusa kulikuwa na tambiko kwa miungu kupitia mizimu kwa madhumuni mbalimbali na hasa walifanya hivyo kwa ajili ya kushukru endapo mwaka mzima hakukuwa na balaa lolote na kuomba msaada kama kuna tukio mfano baa la njaa, magonjwa, ukame ili kutokomeza tatizo hilo. Siku ya tambiko la kuomba mvua ilikuwa ni marufuku kwa mtu yeyote kuwasha moto hasa nyakati za asubuhi hadi pale “Kyungu” (Kiongozi wa matambiko) atakapowasha moto mkubwa kando ya kibanda kidogo maarufu kama “Moto ufya” hii ilikuwa ni kama ishara ya kutoa salaamu za maombi ya mvua kwa mizimu. Waliamini kuwa moto huo ukizimika muda mfupi baada ya kuwashwa basi ombi lao limekataliwa na shughuli za kuomba mvua hubatilishwa hadi siku nyingine.
Katika kufanya hivyo maeneo yaliyohusika kufanyia matambiko yaliitwa “Isyeto/Masyeto, wahusika katika shughuli hiyo walikuwa wazee maalumu, vifaa walivyotumia kutambikia ni pamoja na vibuyu, vyungu, pombe, ulezi, kuku mweusi, pesa. Ng’ombe alichinjwa kwa mwaka mara moja kwenye maeneo hayo ya masyeto kwa kuunganisha na pombe ambapo watu walitumia huko. Mavazi yaliyotumika yalikuwa ni ya kawaida. Katika kutoa sadaka zilitolewa pesa (senti) kila baada ya muda fulani na pombe ambayo kiasi fulani iliachwa kwenye kibuyu, ilikuwa ni marufuku akina mama kutafuta kuni ndani ya isyeto, katika kila isyeto kulikuwa na chifu anayehusika. Katika utambikaji pia kulikuwa na hadhira ambayo ilikuwa ni ya kitaswira yaani mizimu, fanani walikuwa ni wale wazee waliokuwa wanatambika.
Tangu utandawazi umekuwa ukishika kasi kila uchao, dini za kigeni kama Ukristo na Uislamu vimethoofisha sana utambikaji katika “Maganjo na Masyeto”, hii inatokana na watu kuomba mahitaji yao tata katika makanisa na misikiti. Matatizo mengi ya jamii yamekuwa yakielezwa kisayansi na kupatiwa ufumbuzi wa kisayansi, maingiliano ya dini za asili na hizi za kigeni huleta mtafaruku katika jamii na kupunguza mshikamano ndani ya jamii, mfano siku za matambiko, wanajamii hukatazwa wasifanye kazi yoyote ambapo kwa nyakati hizi za utandawazi watu wenye imani tofauti na matambiko huendelea na utaratibu wao kulingana na kile mmoja anavyoamini, hali ambayo huleta pia mtafaruku na migongano katika jamii ambapo pia husababisha kuharibu umoja na mshikamano wa jamii.
Siasa ni itikadi inayofuatwa na kundi au jamii fulani ambayo ni msingi wa kuendesha uchumi, utamaduni na mwenendo mzima wa maisha ya jamii (TUKI, 2004). Katika makabila ya kibantu uongozi katika jamii ulikuwa unapatikana kwa kurithishwa ndani ya ukoo, chifu katika eneo au jamii husika pamoja na viongozi walikuwa wanarithishwa madaraka kutoka kizazi kimoja hadi kingine ndani ya ukoo fulani, kiongozi kabla ya kustaafu alikuwa anamuandaa mtu mmoja katika ukoo wake ili atakapostaafu au kufariki atumie nafasi yake kuuendeleza ukoo. Viongozi katika makabila ya kibantu walikuwa na mamlaka ya kusema lolote katika jamii na kutekelezwa, mfano waliweza kutoa adhabu kwa mtu yeyote yule ambaye alikiuka kaida au taratibu za jamii husika.
Kwa mfano kabila la wasafwa kulikuwa na machifu wengi na kila chifu alikuwa na watu wake wa kumsaidia katika utawala wake hasa wazee wa kimila (Mafumu). Kwa kawaida chifu alichaguliwa kutokana na busara aliyokuwa nayo, uchaguzi haukufuata urithishwaji wa mtoto mkubwa tu, bali ilitazamwa busara aliyokuwa nayo mtoto huyo.
Aliyevunja sheria alipewa adhabu ya kutubu na baadaye kulipa ng’ombe mmoja kwa wazee (Mafumu). Adhabu hii ilikuwa na lengo la kuifanya jamii iweze kuishi katika mwenendo mwema na kuwepo kwa maadili katika jamii hiyo ya wasafwa.
            Ufuatao ni mfumo mzima wa utawala ulivyokuwa katika kabila la wasafwa:
MWENE
                                                         
FUMU MKUU
                                                                                                           
MAFUMU WAKUU
                                                                                                                   
MAFUMU WADOGO          
                                                  

RAIA

Kuingia na kushamiri kwa utandawazi katika makabila ya kibantu kumeharibu mfumo mzima wa uongozi au utawala ambapo kwa sasa viongozi wanapatikana kwa utaratibu wa kiserikali ambao ulitokana na tamko la serikali ya awamu ya kwanza chini ya uongozi wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mnamo mwaka 1963 ambapo alifuta rasmi utawala wa kichifu nchini Tanzania.
Baada ya kufutwa kwa mfumo huu pamekuwepo na mfumo wa vyama mbalimbali vya siasa ambavyo ndio vimekuwa vikigombea uongozi katika ngazi mbalimbali ambapo vimekuwa vikisababisha machafuko ndani ya jamii na kusababisha utengano ndani ya jamii moja ambapo yote haya ni matokeo ya utandawazi.
Uchumi ni mfumo na mapato na matumizi ya watu katika nchi (TUKI, 2004:422). Kwa mujibu wa tafsiri hii uchumi ni mali iliyopatikana kutokana na amali za nchi au watu ambapo hujitengenezea mfumo wao wa mapato na matumizi.
Suala la uchumi katika makabila ya kibantu halikutofautiana katika mifumo ya uzalishaji mali kama vile kilimo, ufugaji, uvuvi na uwindaji kwa kutaja mifano michache. Jamii zilifanya kazi kwa kushirikiana na kugawana mapato kwa usawa. Suala la uvivu lilipigwa vita, hivyo kila mtu aliyekuwa na uwezo wa kufanya kazi alitakiwa awajibike ipasavyo. Shughuli hizi zilienda sanjali na vipengele mbalimbali vya fasihi simulizi kama vile nyimbo, semi na majigambo.
Tukirejea kabila la wanyakyusa kulikuwa na mitindo mbalimbali ya kulima, mkulima mmoja mmoja au kwa kushirikiana katika shughuli nzima ya kulima yaani (Ndimya), ambapo wanakikundi walilima kwa zamu katika shamba la kila mmoja aliyeshiriki katika ushirikiano huu, hivyo walikuwa wakilimiana kwa zamu mpaka mashamba yote yanamalizika. Ingawa wanyakyusa walifanya baadhi ya kazi zao kwa ushirikiano na umoja hawakuwa na jadi ya kuimba wakati wa kufanya kazi zao, badala yake wakati wa mapumziko waliimba nyimbo mbalimbali za maonyo, mafumbo au matukio yaliyokuwa yanatokea katika jamii.


 Mfano wa wimbo ulioimbwa baada ya kazi ni:
                                      “Kiongozi:    Kungwengwelela jumo jwene, jumo fiki fyakwegelaga
                                            wote:        Kungwengwelela jumo jwene, jumo fiki fyakwegelaga”.
Maana yake ni:  “Umempendelea mke mmoja huyo mwingine kitu gani kilikuolea
                              au nani alikuolea?”.
Kwa mfumo huu wa maisha katika jamii za kinyakyusa nyakati za mapumziko baada ya kazi zilikuwa ni nyakati za burudani na kubadilishana mawazo.
Wanyakyusa walihifadhi mazao yao katika ghala zilizojulikana kwa jina la “Mitenene” ambazo zilijengwa kwa matete na kusiribwa kwa kinyesi cha ng’ombe. Pia waliweza kuhifadhi mazao darini ambapo palikuwa ni usawa na mafiga, mazao hayo yaliyohifadhiwa usawa wa mafiga yaliwekwa kwa ajili ya mbegu katika msimu wa kilimo uliofuata.
Baada ya utandawazi kushamiri utaratibu wa kulima umebadilika sana kiutendaji, vifaa vya kutendea na hata namna ya kufanya shughuli nzima ya kilimo, mpaka sasa baadhi ya wakulima walio na uwezo mzuri kiuchumi wanatumia matrekta na plau (Jembe la kukokotwa na wanyama na hasa ng’ombe), wakati huo huo wakulima walio wengi bado wanatumia jembe la mkono ambapo pia wapo wanaolima wenyewe na wengine wanaajiri vibarua kwa ujira wa kutwa au kutegemea na vipimo vya shamba. Kutokana na ubinafsi huo hakuna tena ushirikiano hatimaye kutokomeza matumizi ya nyimbo, semi pamoja na majigambo ambapo hivi vipengele vilisaidia kuleta umoja na mshikamano katika kazi. Pia uhifadhi wa mazao umebadilika sana ambapo kwa sasa nafaka huhifadhiwa kwa kutumia kemikali za kisasa na kuwekwa kwenye maghala ya kisasa pamoja na kutumia mbegu zilizoandaliwa (kisayansi), kisasa zaidi. 

Uhusiano ni hali ya kuwa na fungaman, uhusiano unaweza kuwa mbaya au mzuri (TUKI, 2004:427). Kutokana na maana hii uhusiano ni sehemu ya amali za jamii kwa kuwa ni nyenzo muhimu ya maendeleo katika jamii. Wabantu hutunza uhusiano mzuri baina ya familia, ukoo na jamii kwa ujumla ili kutimiza adhima husika. Mahusiano katika jamii hujidhihirisha katika utani baina ya mtu na mtu, ukoo na ukoo au kabila na kabila. Hali kadhalika salaamu, sherehe, misiba au starehe mbalimbali zilikuwa ni ishara ya mahusiano mazuri katika jamii.
Wanyakyusa wamegawanyika katika makundi makuu mawili kulingana na hali ya kijiografia, kuna wale wanaoishi bondeni yaani “Ntebela” hususani pwani ya ziwa Nyasa wenyewe huita “Nyanja” kwa maana ya bahari na wengine huishi milimani. Mgawanyo huo wa kijiografia umesababisha tofauti kubwa kiuchumi. Wanyakyusa wa bondeni ambayo ni wilaya ya Kyela wanajishughulisha na kilimo cha mpunga pamoja na mazao mengine wakati hawa wanyakyusa wa milimani hujishughulisha zaidi na kilimo cha ndizi na aina nyingine ya mazao yaliyo katika mfumo wa mizizi iliwayo. Hata hivyo kutokana na mahusiano mazuri kati yao waliweza kubadilishana bidhaa, mara nyingi wale wa milimani walibeba magimbi, ndizi na hata mahindi ili kubadilishana na mpunga au samaki hali iliyozua utani na nyimbo kati yao. Wanyakyusa wa bondeni walikuwa wanaimba nyimbo kama:
                       “Kiongozi  :  Bisile aba mwamba aba ngata inywamu
                              wote    :  Bisile aba mwamba aba ngata inywamu
                         Kiongozi   : Sokamo mu mphulo gwe kapimba ugwe
                              wote     : Sokamo mu mphulo gwe kapimba ugwe”.
Maana yake ni;     “ Wamekuja watu wa milima
                                 wenye nzinga kubwa
                                 ewe kajitu kafupi ondoka uwanjani”.
“Nzinga kubwa” ilitumiwa na wanyakyusa wa milimani ili kupunguza msuguano kichwani kutokana na uzito wa mizigo waliyoibeba kichwani. Mabadilishano ya biashara yalionesha uhusiano mzuri na kujenga undugu kati yao. Pia misemo ya utani kama vile  “Aba ngulya gwene” ulikuwa ni msemo uliomaanisha kwamba watu wa milima ambao wanaweza kula wali bila mboga. 
Katika kabila la Wanyakyusa na Wasafwa wana namna moja katika kushirikiana wakati wa misiba na matatizo mbalimbali kwa mfano, ukitokea msiba katika familia fulani kwenye jamii, jamii nzima huhusika katika msiba ule na kushirikiana katika shughuli zote za msiba huo. Wanaume na wanawake wa jamii nzima waliwajibika kushinda na kulala mahali palipotokea msiba na kila mmoja katika jamii huweza kuchangia chakula, kuni na vifaa vingine vilivyotumika katika shughuli nzima ya mazishi kama vile majembe, makoleo, mkeka na ng’ombe, hii ilikuwa ni kulingana na uzito wa msiba uliokuwa umetokea. Mbolezi ziliimbwa wakati wote wa msiba ambapo waghani walikuwa wakitaja sifa na mema ya marehemu au ukoo wa marehemu, waombolezaji wengine waliimba na kupita sehemu mbalimbali za makazi yao wakiimba na kuchangishana nafaka kwa ajili ya msiba, kwa mfano katika kabila la Wasafwa walikuwa wanaimba nyimbo kama hizi:
                                       “Kiongozi:     Ndio maana ×2
                                        Waitikiaji:   Ndio maana twinzile      
                                        Kiongozi:     Ndio maana ×2
                                        Waitikiaji:   Ndio maana twinzile
                                        Kiongozi:     (Hutaja jina la marehemu au ukoo wake)
                                        Waitikiaji:   Ndio maana twinzile”.
Wimbo huu hutumika kuonyesha uhusiano mzuri kati ya jamii na ndugu pamoja na jamaa waliofiwa, wimbo una maana kuwa (Tumekuja kwa sababu tunaushiriano na nyie).
Kwa upande wa kabila la Wanyakyusa waliimba hivi:
                                       “Kiongozi:   Twalimenye naloli           
                                        Waitikiaji:  Twalimenye naloli
                                         Kiongozi:   Ukete abhandu bikulila
                                         Waitikiaji: Ukete abhandu bikulila
                                         Kiongozi:  Keta tukwenda tukulila
                                         Waitikiaji: Keta tukwenda tukulila”
Wimbo huu ulikuwa na maana kwamba kulikuwa na uhusiano mzuri kwa kusema:
                                       “Kiongozi:  Tulimjua sana       
                                        Waitikiaji: Tulimjua sana
                                        Kiongozi:   Ona watu wanavyolia
                                        Waitikiaji:  Ona watu wanavyolia
                                        Kiongozi:   Tazama tunatembea tukilia
                                        Waitikiaji:  Tazama tunatembea tukilia”.
Kutokana na utandawazi kuingia katika jamii hizi fasihi simulizi iliyotumika kama amali ya mahusiano imepoteza uasili wake katika kuihifadhi, kuwasilishwa, muktadha wake pamoja na maudhui. Katika kipindi hiki cha utandawazi nyimbo kama hizi za mbolezi zimerekodiwa katika kanda na zinaweza kuimbwa popote na wakati wowote bila kuzingatia muktadha na katika hali yoyote. Kutokana na athari hizo za utandawazi uhusiano katika jamii umedhoofika, kwa mfano mtu anaweza kununua kanda na kwenda kusikiliza nyumbani, hivyo kwa sasa hata nyimbo hizi kwenye misiba huwa zinawasilishwa kwa kutumia kanda za muziki na hivyo kupoteza uhalisia wake.

Jando na unyago ni sehemu ya malezi inayolenga kumsaidia mtoto kukabili vema hali yake ya kuwa mwanaume au mwanamke ili jinsia imjenge badala ya kumvuruga. Mara nyingi wavulana huwa wanaongelea sri zao zinazowahusu wao katika makuzi yao na huwa hawataki mtoto wa kike kuzijua hali kadhalika kwa upande wa mtoto wa kike nao huwa wanamafunzo yao ambapo nao huwa hawapendi mambo wanayojifunza yajulikane kwa watoto wa kiume, mafunzo haya yaliweza kutolewa na watu wazima ambao ndio walitegemewa zaidi na jamii katika kutoa elimu ya jinsia.
Katika jamii za kibantu zilikuwa na kawaida ya kuongelea mafunzo hayo ya siri na wazee hasa babu na bibi ndio walihusika sana katika kutoa mafunzo hayo, kulikuwa na mafundisho rasmi ambayo yalikuwa na umuhimu wa kujua mapema ukweli hasa kuhusu maumbile ya binadamu. Kadri mtoto anavyozidi kukua ndivyo alivyohitaji kujifahamu kijinsia ili aweze kukomaa na hatimaye kukabiliana na shughuli mbalimbali za kijamii.

Katika kabila la Wanyakyusa walizingatia malezi ya vijana na ilikuwa ni mwiko kwa mtoto wa kinyakyusa kudeka, mama aliweza kula na watoto wa kiume chini ya miaka kumi pamoja na wale wa kike ambao walikuwa bado hawajaolewa, lengo kubwa ilikuwa ni kuwafundisha kula kwa adabu na kuheshimiana. Kwa upande wa mtoto wa kiume aliruhusiwa kukaa na mama yake akiwa na umri chini ya miaka kumi, baada ya umri huo hakuruhusiwa kukaa tena na mama yake bali aliambatana na wanaume kwa lengo la kujifunza kazi. Mgawanyo wa kazi ulizingatia umri na jinsi kwa kuwa zamani watoto wengi hawakuwa na fursa za kusoma, hivyo walipata elimu (mafunzo) kutoka kwa wazazi wao. Watoto walipofikisha umri wa miaka kumi na moja au kumi na mbili waliweza kukusanywa kutoka familia tofauti na kupelekwa mbali na wazazi wao ili kujifunza maisha na kujitegemea na hivyo kuweza kuanzisha vijiji vipya kwa kujenga nyumba kisha kuanzisha familia.
Wakati wa utoaji wa mafunzo hayo semi na nyimbo mbalimbali zilitumika na zilitolewa na wazee, kwa mfano:
                                           “ Ukukoma ingunguni”
             Tafsiri yake ni;        “Kuua kunguni” 
Msemo huu ulilenga kuelimisha watoto na kuwakomaza kuwa kuendelea kuishi kwenye nyumba ya wazazi pamoja nao na hali wakiwa wamefikia umri wa kujitegemea sio vizuri, hivyo walisisitizwa zaidi kujitegemea. (Mwambusye, 2012:23).
                                              “Ukukula kitalikitali”
             Tafsiri yake ni;        “ Kukua haraharaka lakini bila umbile na akili au hekima”.
Katika msemo huu walimaanisha zaidi kuwa mwili unakua upesi kuliko akili yaani ukuaji wa mwili hauendi sambamba na ukuaji wa akili ( Mwambusye, 2012:27).
Kutokana na mafunzo haya ya kukaa pamoja, vijana waliweza kujifunza majukumu mbalimbali na malezi ya jamii zao kwa ajili ya maendeleo ya pamoja na kuhimiza ushirikiano, kuheshimiana na kuthaminiana na hatimiye kuishi kama ndugu na jamii moja na hapo ndipo  Wanyakyusa wanapo sema:
                                            “Nkamu ju mundu”
                 Tafsiri yake ni:   “Undugu ni kufaana na sio kufanana”.
Kutokana na kushamiri kwa utandawazi, mfumo huu wa maisha umeathiriwa kwa sababu muda mwingi watoto wanakuwa shuleni na wanapofikia hatua ya kuhitimu elimu ya msingi huwa katika umri wa miaka kumi na tatu hadi kumi na sita na baada ya hapo wengine hubaki kijijini na wengi huweza kuhamia mijini.
Pamoja na hayo, hata kule vijijini hakuna tena ardhi ya kutosha kuanzisha vijiji vipya kama ilivyokuwa zamani na hii imesababisha iwe vigumu kupata nafasi ya kuhudhuria mafunzo au malezi ya kijamii.
Kwa upande wa kabila la Wasafwa, mtoto alipewa elimu kwa vitendo ambapo elimu ya kwanza kabisa kwa mtoto wa kisafwa ni elimu ya kilimo, mtoto wa kiume na wa kike akifikia umri wa miaka mitano na kuendelea alifundishwa kuwa jembe ndio kila kitu, jembe ndio maisha yake, aliweza kupewa sehemu ndogo ya shamba kwa ajili ya kulima mahindi ya kuchoma, alitengenezewa jembe dogo la mpini mfupi kadri ya kiganja chake cha mkono, hivyo alifundishwa namna ya kuwasaidia wazazi wake. Mtoto wa kiume pia alifundishwa elimu nyingine na ilitolewa kulingana na kazi aliyopendelea kuifanya atakapokuwa mkubwa, mfano alifundishwa kujenga nyumba, kuchonga mizinga ya nyuki, kukamua maziwa ya ng’ombe, mbuzi na kondoo. Pia alifundishwa namna ya kuishi na mke. Kwa upande wa mtoto wa kike naye hakuwekwa mbali na mafunzo ya kumuimarisha zaidi atakapokuwa mkubwa ambapo alifundishwa kupika, kusafisha vyombo na nyumba pamoja na namna ya kuishi na mume pamoja na namna ya kulea watoto.
Hakukuwa na elimu ya marika, bali watoto wa jinsi zote waliweza kula pamoja, kucheza na kulala pamoja na watoto wengine katika jamii. Wakati wa kula, kama mtoto amesimama wima ikiwa wengine wamekaa aliambiwa aende nje amwite “Mwimilila” yaani aliyesimama, basi mtoto huyo ataita kwa sauti akiwa hajui kama anajiita yeye mwenyewe. Kwa upande wa maonyo vilitumika vitendawili kama “Inzili nu mwene” yaani sina mfalme, ambapo waitikiaji walijibu “Ulundyelele” kwa maana ya utelezi wakilenga kufafanua kuwa utelezi hauchagui mtu unaweza kumdondosha mfalme, tajiri hata masikini. Katika maisha ya sasa kitendawili hiki kingeweza kutumika kuonya watu wawe makini na tabia zao maana kuna magonjwa hatari yasiyochagua wa kubagua kama vile “Ukosefu wa Kinga Mwilini” (UKIMWI).
Kutokana na maendeleo ya utandawazi katika harakati za kupambana na maisha jamii ya Kisafwa imetawanyika na kujikita zaidi katika shughuli za watu wa makabila mengine kama vile biashara, ulinzi na hata shughuli za udereva. Ni vigumu kwa vijana wa sasa wa kisafwa kuelekezwa kuwa shughuli kuu katika kabila lao (kisafwa) ni kilimo na wakaelewa, hii inatokana na kuwa wengi wao wamesoma na hivyo kuona kuwa kukimbilia mjini na kuendelea na shughuli zingine kama biashara, kazi za ofisini tofauti na zile za jamii yao ni ufahari na hivyo kuendelea kuishi mijini na kudharau vijijini pamoja na shughuli za kilimo na hivyo kuona shughuli hiyo imepitwa na wakati.
Afya ni kuwa na hali nzuri ya mwili bila ya maradhi, uzima, siha (TUKI, 1981). Kwa ujumla afya ni hali ya kutunza mazingira kwa lengo la kumtunza binadamu asipatwe na maradhi yoyote ya kimwili ikijumuisha utunzaji wa vyanzo vya maji, masuala ya tiba, uzazi wa mpango na upatikanaji wa chakula bora. Jamii mbalimbali za kibantu zimekuwa zikitunza afya zao katika nyanja mbalimbali kama vile masuala ya tiba, maji, uzazi wa mpango na chakula bora kwa ajili ya maendeleo mbalimbali katika nyanja za kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na mengineyo.
Katika makabila ya kibantu afya ilionekana kama ndio msingi wa maisha yao. Pia afya mbovu ilionekana kama kichocheo hasi cha maendeleo, ili jamii iepukane na maradhi hayo ilitumia tiba mbalimbali za asili, mfano kwa upande wa wanyakyusya walizingatia sana utunzaji wa vyanzo vya maji ambapo maji hayo yalitumika kwa ajili ya kupikia na kunywa, maji ya kunywa yalitokea katika chanzo chake kutoka kwenye mwinuko wa chanzo hicho na yalitiririka kupitia kifaa maalumu kilichijulikana kama “Lyubhubhu”,ambalo ni ganda la mgomba au bomba lenye uwazi mkubwa. Sehemu hiyo haikuruhusiwa mtu yeyote kuoga wala kufua na kufanya shughuli zingine zaidi ya kuchota maji tu, ilifanyika hivyo ili kutunza maji na vyanzo vyake, hivyo basi kuna sehemu zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya kuoga na kufulia ambapo zilikuwa mbali na zile za kuchota maji. Tiba za dawa za asili zilitumika kwa kuponya au kuzuia magonjwa yaliyojitokeza katika jamii ya kinyakyusa, kulikuwa na dawa ya kutibu magonjwa mbalimbali kwa mfano “Pupwe” ni dawa ya kutibu tumbo, “Kibangula” ni dawa ya mafua, “Mingongobhele nsemwasemwa” hii ilitibu tumbo na kisukari. Pia kulikuwa na dawa ambazo ziliandaliwa na watu maarufu, hizi zilinyunyizwa kwenye mlango wa kila nyumba ili kuondoa balaa au kuzuia balaa kama magonjwa. Kitendo cha kunyunyiza kilijulikana kama “Kumisa” yaani kutoa balaa.
Wanyakyusa pia walitumia uzazi wa mpango kwa kutumia njia mbalimbali za asili ambazo hazikuwa na madhara yoyote katika miili yao, mfano wanawake walivaa dawa kiunoni ili kuzuia mimba na kuepuka kuzaa watoto wa kufuatana kwa mfululizo na kwa muda mfupi. Njia nyingine mwanamke (mzazi) alipelekwa kwa wakwe mpaka mtoto atakapokuwa na umri mkubwa  kiasi cha kumuwezesha tena mama mzazi akipata ujauzito mwingine isilete madhara katika malezi ya mtoto aliyepo. Njia hizi zote zilisaidia kupata idadi ya watoto wanaotakiwa au idadi iliyopangwa na familia husika, pia kuipa familia nafasi ya kulea mtoto aliyezaliwa.
Kulingana na utandawazi, tiba na kinga hufanyika kwa kutumia dawa za kutibu na kukinga magonjwa mbalimbali kama vile panado, septrini, kinga za kifaduro, polio, surua na mengine mengi, kwa upande wa uzazi wa mpango kumekuwepo na vidonge vya majira, vitanzi, sindano za kuzuia mimba pamoja na mipira ya kiume na kike. (Kondomu).
Kwa upande wa kabila la wasafwa, usafi wa nyumba, mwili ulitiliwa mkazo na kuwa na umuhimu mkubwa hasa kwa wanawake. Nyumba zao zilisilibwa kwa udongo wa rangi mbalimbali na kuchorwa michoro ya urembo tofauti tofauti. Mavazi yao ambayo yalikuwa ni ngozi za mbuzi zilizolainishwa kwa mafuta ya ng’ombe au mafuta ya nyonyo yalitunzwa kwa uangalifu. Kabila hili la wasafwa kama walivyo wanyakyusa walioga ndani ya vijito ambavyo huzunguka makazi yao kwani wasafwa huweza kuweka makazi yao karibu na vijito. Jamii ilikemea uchafu wa mwili kwa kutumia mafumbo pamoja na nyimbo mbalimbali, kwa mfano moja ya nyimbo zilizotumiwa kuhimiza utunzaji na usafi wa mwili kwa kuoga ni pamoja na:
                             “Uyogaje  uyogaje × 2
                             uyogaje hyena muzina uyogaje
                             Ihwili isabuni ya sumuni uyogage”.
Maana yake ni:  “Uwe unaoga, uwe unaoga
                             mama mtoto uwe unaoga
                             sasa kuna sabuni ya thumuni”.      
Suala la maji, katika jamii ya kisafwa ilitunza vyanzo vya maji, hasa yanayotumika kupikia na kunywa. Ilizuiliwa kunywesha mifugo au kukanyaga penye chanzo cha maji, maji mengi hutiririka kutoka milimani ambapo wasafwa huita “Inzalala” kwa maana ya maji yanayotiririka.
Kutokana na maendeleo ya utandawazi  siku hizi wasafwa hutumia maji ya bomba, tiba za kisasa na kusababisha dawa za asili kukosa umaarufu na umuhimu. Hivyo dawa za kisasa zina madhara makubwa tofauti na zile za asili ambazo zilikuwa ni za uhakika na zilisababisha watu wa jamii hii kuweza kuishi muda mrefu bila matatizo.
Kukua kwa sayansi na teknolojia ni sehemu muhimu sana katika kuleta maendeleo katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni ambapo maendeleo ya sayansi na teknolojia yamesababisha utandawazi. Kutokana na mabadiliko haya, fasihi simulizi kama kazi ya kisanaa iliyojaa ufundi na ubunifu ndani yake haina budi kuendana na mabadiliko hayo maana hata mfumo wa maisha hubadilikabadilika katika jamii kulingana na maendeleo yanavyozidi kuimarika na kujitokeza. Hivyo pamoja na mabadiliko hayo si vyema kupuuza fasihi simulizi kwani yenyewe ndiyo fasihi kongwe na ndiyo iliyoibua fasihi andishi baada ya kugundulika kwa maandishi kwani fasihi hata kabla ya utandawazi ilikuwa na mchango mkubwa sana katika kuimarisha amali za jamii.

MAREJEO
Balisidya, M. L, (1983), Tanzu na Fani za Fasihi Simulizi, kutoka kwa Mulika namba 19 (1987),
                                     Taasisi ya Uchunguzi  wa Kiswahili, Chuo Kikuu Dar es Salaam.

Mulokozi, M.M (1996), Fasihi ya Kiswahili, Dar es Salaam, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.
Mwanbusye, D (2012), Lugha, Utamaduni na Fasihi simulizi ya Kinyakyusa, Dar es Salaam.
Ngure, A (2003), Fasihi Simulizi kwa Shule za Sekondari, Nairobi, Phoenix Publishers Ltd.

Finnegan, R. (1970), Oral Literature in Africa, OpenBook Publishers, Cambridge.
TUKI, (1981), Kamusi ya Kiswahili Sanifu, Nairobi, Oxford University Press Ltd.

TUKI, (2004), Kamusi ya Kiswahili Sanifu, Dar es Salaam, Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili.

No comments:

Post a Comment