Saturday, 22 March 2014

OSW 226. USHAIRI WA KISWAHILI BY. MWL. JAPHET MASATU

OSW  226. USAHAIRI  WA   KISWAHILI.


    WANA MAMBOLEO NA WANA MAPOKEO

     WANATOFAUTIANAJE KATIKA KUELEZA 

       MAANA  YA USHAIRI WA KISWAHILI?

 Wataalamu mbalimbali wameeleza maana ya ushairi wa kiswahili, lakini mawazo yao yamefungamana katika sehemu fulani na kuofautiana katika baadhi ya maeneo. wataalamu karibu wote yaani wale wa kimambo leo na kimambo kale kwa pamoja wanaamini kuwa shairi lazima liwe na:

  •  mpangilio mzuri wa maneno
  • lugha inayoeleweka
  • lenye kuleta maana kwa hadhira iliyokusudiwa
 vile vile wataalamu hawa wa kimamboleo na kimambokale wanatotautiana katika baadhi ya maeneo. maeneno hayo ni pamoja na:
  • mpangilio wa urari wa vina na mizani
  • mabeti
  • kibwagizo au bahari
 ZIFUATAZO NI MAANA ZA USHAIRI KULINGANA NA MAWZO YA WANA MAPOKEO
Shaaban Robert katika Massamba (1983:55) anasema :
                         “Ushairi ni sanaa ya vina inayopambanuliwa kama nyimbo, mashairi na tenzi.
                          Zaidi ya kuwa sanaa ya vina, una ufasaha wa maneno machache au muhtasari.
                          Mwauliza wimbo, shairi na tenzi ni nini? Wimbo ni shairi ndogo, ushairi ni
                          wimbo mkubwa na utenzi ni upeo wa ushairi. Mwauliza tena kina na ufasaha
                          huweza kuwa nini? Kina ni mlingano wa sauti za herufi. Kwa maneno mengine
                          huitwa mizani ya sauti na ufasaha ni uzuri wa lugha. Mawazo na maoni na
                          fikra za ndani zinapoelezwa kwa muhtasari wa shairi huvuta moyo kwa namna
                          ya ajabu”.
Naye Abdilatifu Abdalla katika Massamba (1983:57) anasema:
 “Utungo ufaao kupewa jina la ushairi si utungo wowote bali ni utungo ambao  katika kila ubeti wake kuna ulinganifu wa vina vitukufu vilivyopangwa kimoja baada ya chenziye, wenye vipande vilivyo na ulinganifu wa mizani. Na vipande  hivyo viwe vimetandwa na maneno ya mkato maalum na yenye lugha nyoofu, tamu na laini. Lugha ambayo ina uzito wa fikra, tamu kwa mdomo wa kusema, tumbuizi kwa masikio ya kusikia na yenye kuathiri moyo uliokusudiwa na kama  ilivyokusudiwa”.
Mayoka (1986:3) anasema:
 “Ushairi ni mtungo wa kisanaa ulio na mpangilio maalum wa lugha ya mkato ambayo ndani yake ina vina, urari wa mizani na muwala maalum ambavyo kwa pamoja huwa na fani na maudhui yahusuyo hisi fulani au tukio juu ya maisha ya  mtu au watu wa mazingira na wakati maalum”.
WANA MAMBO LEO
Wangari na Mwai (1988:5) wanaonesha kuwa washairi wa kisasa wanaeleza kwamba fasihi hubadilika katika umbo na maudhui na kwa hiyo ushairi wa Kiswahili sharti uruhusu mabadiliko yanayotokea katika ushairi huru.
 Mulokozi na Kahigi (1979:25) wanasema:
 “Ushairi ni sanaa inayopambanuliwa kwa mpangilio maalum wa maneno fasaha yenye muwala, kwa lugha ya mkato, picha au sitiari katika usemi, maandishi, au mahadhi ya wimbo ili kueleza wazo au mawazo, kufunza au kueleza tukio au hisi fulani kuhusu maisha au mazingira ya binadamu kwa njia inayogusa moyo”